Yanayojiri wikendi

Huku mwisho wa juma unapojongea, ni wazi kuwa kila mtu ana mipango yake anayopania kutekeleza na kujipa mapumziko baada ya juma lenye shughuli si haba. Katika harakati hizi, shirikisho la magongo nchini KHU halijasazwa katika mipango yake ya kuwapa mashabik burudani si haba. Takriban mechi kumi na sita zitasakatwa kati ya jumamosi na jumapili katika maeneo tofauti nchini.

Burudani itang’olea nanga jijini Nairobi na dimba la daraja la pili la ligi ya akina dada. Mchuano huu utakuwa baina ya mabinti wa chuo kikuu cha Multimedia watakapowaalika vidosho kutoka Nakuru. Wawili hawa wanawania kuzoa alama tatu muhimu na kupiga jeki matumaini yao ya kupanda hadi ligi kuu ya akina dada chini. Baadae itakuwa zamu ya chuo kikuu cha Kiufundi nchini Technical University of Kenya kujitosa ugani na kuwania kutia doa katika mbio za Wolverines za kuwania kujiunga na ligi kuu. Wolverines ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya kwanza katika jedwali la ligi hio, watakuwa mbioni kutumia ubabe wao katika mchezo na pia maarifa ya wakufunzi wao kuichabanga TUK vilivyo.

Wapenzi wa magongo katika maeneo ya pwani nao pia watakuwa na kila sababu ya kutabasamu pale ambapo klabu ya akina dada ya Mombasa Sports Club upande wa akina dada itakapoialika chuo kikuu cha Nairobi. Akina dada wa Pwani watatumia uzoefu wao wa hali ya hewa huko na kutarajia kusalia na alama tatu muhimu huku vidosho wa Nairobi wakijikaza baada ya kuandikisha matokeo duni katika mchuano wao wa juma lililopita.

Katika upande wa wanaume, kivumbi kitachimbika kote nchini katika daraja zote tatu. Katika ligi ya kitaifa, itakuwa zamu ya chuo kikuu cha Eldoret almaarufu UoE chini ya ukufunzi wa Collins Cheloti na Emmanuel Kongin kuialika Thika Rovers mjini Eldoret. UoE itakuwa mbioni kujipa ushindi haswaa baada ya kuandikisha matokeo duni katika mkondo wa kwanza wa ligi.

Mjini Kisumu, klabu ya Kisumu Youngstars inatarajia kuwapa wapenzi wa magongo sababu za kutabasamu kwa kutwaa ushindi dhidi ya vijana wa TUK. Licha ya hii kuwa mechi ambayo itakuwa na upinzani mkali, Youngstars watatumia ile dhana ya kuwa nyumbani na matokeo ya mechi yao dhidi ya Nakuru wikendi iliyopita.

Katika kaunti ya Bungoma, Bungoma Farmers watakuwa na kibarua cha ziada pale watakapo chuana na wahasibu KCA. Farmers ambao wamekuwa na msimu usio wafaa, wanafahamu fika kuwa njia ya pekee ya kuzuia shoka ya shirikisho na kurejea katika ligi ya kitaifa, ni kwa kuanza kuandikisha ushindi. KCA nao kwa upande wao, wanawania kuendeleza msururu wa matokeo bora na kuangazia kupanda daraja. Mjini Nairobi, wasomi wa kiume wa chuo kikuu cha Multimedia watawaalika wawakilishi wa wapwani Mvita. Mvita ambao wanajivunia kuwa na wachezaji wenye ujuzi mwingi katika mchezo huu kunykua ushindi.

Katika ligi kuu Western Jaguars inajiandaa kuialika Parklands Sports Club katika mechi ambayo wote wanatarajia kuibuka na ushindi. Jaguars watawania kushinda mechi hii ya mkondo wa pili baada ya kuicharaza Parklands katika mechi ya mkondo wa kwanza. Kwa upande wao, Parklands wanawania kutwaa ushindi na kuepuka hatari ya kushushwa daraja na pia kuwa timu ya tatu kuicharaza Jaguars kwao nyumbani baada ya Kenya Police na Butali Warriors. Kwa upande wao, Jaguars wanaangazia kumaliza msimu huu wakiwa katika nne bora na kubadili hali ya hapo awali ambapo walikuwa wanaponea shoka la kushushwa daraja kwa bahati tele.

Mchuano mwingine unaosubiriwa kwahamu ni ule kati ya Sailors na Wazalendo. Baada ya kupoteza mechi dhidi ya chuo kikuu cha Strathmore Jumapili iliyopita, Wazalendo wanaendelea kunoa makali yao tayari kuwa tia doa Sailors. Sailors nao wanaangazia kutwaa ushindi na kuendeleza matokeo ya Wazalendo kuwa mabaya.

Mechi za Jumapili ni kama zifuatazo

Impala vs Mvita                                    9:00                 Nairobi

MMU-Women vs Oranje                      11:00               Nairobi

KU-Men vs Parkroad Badgers               13:00               Nairobi

USIU-A women vs Sliders                    15:00               Nairobi

USIU-A men vs Butali                          17:00               Nairobi

Bungoma Farmers vs TUK-Men            10:00               Bungoma

Juma litafika tamati siku ya Jumapili jioni kutakapo andaliwa mechi ya ligi ya waliobobea na kustaafu Masters League. Mechi hio itakuwa baina ya Sikh Union na Parkroad veterans.

Kutoka kwa kikosi kizima cha Magongo Kenya, Tunawatakia wikendi yenye burudani si haba nasi tutaendelea kukujuza yanayojiri katika mechi zote na Matukio kadri yanapochipuka

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *