Msimu 2020 wang’oa nanga

Katika ile hali ya kuazimia kumaliza msimu mapema na kuzipa timu zitakazo shiriki katika mashindano ya kombe la klabu bingwa barani Afrika mwishoni mwa mwaka wakati mwafaka wa kujitayarisha, shirikisho la magongo nchini limekata kauli ya kuwa na mechi moja katikati mwa juma ili kuafiki lengo hilo. Kwa kuwa Subira huvuta heri,  hatimaye zamu ya Parkroad Tigers ambao walinyakua nafasi ya pili mwaka jana katika ligi ya kitaifa na kupata kupanda daraja, watajitosa ugani kuchuana na klabu ya Parklands Sports Club ambao walishushwa daraja kutoka ligi kuu hadi ligi ya daraja la pili.

Kwa upande wao, wenyeji katika mchuano huu Parklands watatizamia kujizoa na kutikisa vumbi huku lengo lao likiwa kunyakua alama tatu na kutangaza uwepo wao. Parkroad nao hawasazwi kwani wao pia wanaangazia kutwaa ushindi katika mechi yao ya kwanza na kutangaza kuwa hawakubahatika tu kupanda ngazi.

Itakuwa kibarua kigumu kwa vikosi hivi vyote kwani mmoja ana doa ambalo yuataka kufuta naye mwingine yuaangazia kubaki bikra msimu wao unapoanza.

Vile vile vikosi vyote hivi vina ufuasi si haba na wafuasi wao pamoja na washika dau wanatarajia kupata jambo la kujivunia.

Kwa upande wake, shirikisho la mchezo wa mpira wa magongo nchini KHU linazidi kujivunia uwezo wao wa kuandaa mechi haswaa baada ya kongamano la marefa na maafisaa wanao simamia mechi. Hii ni katika ile hali ya kuimarisha na kuwapa marefa motisha ya kuangazia kujumuishwa katika marefa wa shirikisho la magongo barani na vile vile duniani ambapo ni wakenya wachache wakiwemo Peter Obalo, Tina Agunda, Tony Fernandez na Bi. Caren kwa sasa.

Vile vile, ujio wa timu mpya utaipa kila kikosi azma ya kuangazia kupandishwa daraja na kuzifanya vitengo vyote kuwa na upinzani mkali wenye kusisimua.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *