Maangazio ya wikendi

Huku mwaka na msimu wa magongo nchini unapo endelea kusongea utepe, mashabik wa magongo nchini wanazo kila sababu ya kujumuika pamoja katika nyuga za magongo katika maeneo tofauti ili kushabikia vikosi vyao vitakapo kuwa vinachuana.

Siku ya Juma mosi mida ya saa sita mchana, itakuwa zamu ya wasomi wa chuo kikuu cha Kenyatta (K.U) kuwaalika Amira katika mechi ya marudio. Amira wanaangazia kuendeleza msururu wa matokeo bora kwa kuwapa kichapo wanafunzi hao haswaa baada ya kuwacharaza wasomi wa chuo kikuu cha USIU-A wiki mbili zilizopita. Mkufunzi wa Amiras Thomas Mucheni ana imani kuwa kikosi chake kimenoa makali yake vilivyo tayari kuwakabili K.U katika mechi ya ligi kuu ya akinadada.

Baada ya mechi hii, itakuwa zamu ya ligi ya daraja la pili pale ambapo klabu ya Vikings chini ya ukufunzi wa Clyde Mmbaha kuwaalika wanadada toka Pwani, Mombasa Sports Club. Baada ya vikosi hivi kupoteza mechi zao dhidi ya chuo kikuu cha Nairobi, wote wanaangazia kuzoa alama moja au tatu katika mechi hii na kuimarisha matumaini yao ya kupandishwa daraja hadi ligi kuu ya wanawake msimu ujao.

Katika upande mwingine wa ukurasa, ligi ya kitaifa upande wa wanaume pia haijasazwa. Wapenzi wa magongo mjini Eldoret watapata fursa ya kutumbuizwa pale ambapo vijana wa chuo kikuu cha Eldoret chini ya babe wa magongo Collins Cheloti na Emmanuel Kongin watakuwa wenyeji wa wenzao wa Mount Kenya University kutoka Thika. Timu hizi mbili hazijakuwa na matokeo ya kuridhisha vile na hii ni fursa ya wao kujitahidi na kuangazia ushindi.

Katika ligi ya daraja la pili upande wa wanaume, kumeratibiwa kugaragazwa mechi mbili za kukata na shoka siku ya Juma Mosi. Wapenzi wa magongo mjini Kisumu na viungani vyake watapata fursa ya kuwashabikia vijana wao Kisumu Youngstars watakapo waalika KCA-U. Youngstars wanaazimia kutia doa katika matokeo ya KCA-U hasa baada ya kuichabanga Impala kwa mabao matatu kwa moja mjini Nairobi juma lililo pita. KCA kwa upande wao, KCA wanawania kuendelea kuangaza moto wao na kutizamia kupanda daraja kurudi ligi kuu ya wanaume mwaka ujao. Vile vile, mjini Nairobi, chuo kikuu cha Kenyatta kitaialika Wazalendo Masters mwendo was saa kumi adhuhuri katika mechi yao ya marudio. Kenyatta wanaangazia kujitikisa vumbi baada ya kupoteza mechi yao ya mwisho na kutwaa upinzani mkali kama vile walivyoishangaza Parkroad kwa kuzoa sare baada ya kupoteza mkwaju wa penalti.

Siku haitakamilika katika ulingo wa magongo kabla ya mechi ya ligi kuu ya wanaume kusakatwa. Baada ya kupoteza mechi yao dhidi ya Western Jaguars mjini Kakamega, itakuwa zamu ya Wazalendo kuwaalika vijana wa ‘Ingo’. Huku vikosi hivi vikijivunia kuwepo kwa vijana barubaru katika vikosi vyao na pia ukuzaji wa talanta na ubabe katika mchezo huu, mechi hii inatarajiwa kuwa kali mno kwani wote hawa wanatizama kumaliza msimu huu katika tatu bora. Licha ya kutokuwepo kwa wachezaji kadhaa kutokana na jeraha au usafiri nje ya nchi, wakufunzi wote wanaimani kuwa wataibuka na ushindi au sare.

Ratiba yamechi za Juma Mosi

Ligi Timu Saa Uga
PLW KU-Women vs Amira 12:00 City Park
SLW Vikings vs MSC-Women 14:00 City Park
NLM U.o.E vs MKU 15:00 Eldoret
SLM Kisumu Youngsters vs KCA-U 15:00 Kisumu
SLM KU-Men vs Wazalendo Masters 16:00 City Park
PLM Wazalendo vs Western Jaguars 18:00 City Park

Siku ya jumapili itakuwa na burudani si haba. Siku itaanza mida ya saa tatu na mechi ya ligi kuu ya wanaume pale ambapo itakuwa ni zamu ya walinda usalama nchini, Kenya Police kuwa wenyeji wa vijana wa ‘Ingo’, Western Jaguars. Katika mkondo wa kwanza, Police waliibuka na ushindi na watawania kutwaa ushindi tena huku Jaguars ikiangazia kubadili matokeo hayo.

Mjini Bungoma, wenyeji Bungoma Farmers watawaalika KCA-U katika mechi ambayo mvua ilikatiza mechi mnamo tarehe 14 mwezi uliopita. Farmers ambao wanaandamwa na jinamizi la kushushwa daraja, watakuwa mbioni kutafuta ushindi ili kuimarisha matumaini yao ya kusalia katika ligi ya daraja la pili.

Tukirejea Nairobi, safari ya akinadada wa MSC mjini Nairobi itakamilika wakati watakapochuana na wenyeji wao kutoka chuo kikuu cha kiufundi cha Nairobi TUK. Mechi hii inapewa upato kuwa mechi ya kusisimua kwani TUK watatumia ujana wao kutafuta ushindi huku MSC ikitumia ueledi wao kwenye mchezo huu wakijumuisha ujana wa baadhi ya wachezaji wao ili kunyakua alama tatu muhimu.

Klabu ya Nakuru ambayo kwa upande wao wamekuwa na mchanganyiko wa matokeo msimu huu watakuwa ugani kuchuana na wenyeji wao ambao ni wasomi wa chuo kikuu cha maswala ya mawasiliano Multimedia University mwendo was aa saba mchana. Wawili hawa wanatizamia ushindi kwani ushindi katika mechi hii utamuona mshindi akipanda katika msimamo wa jedwali. Baadae itakuwa zamu ya ligi kuu ya akinadada pale ambapo itakuwa mchuano kati ya vidosho wa KU, dhidi ya wale wa JKUAT. Mshindi katika mechi hii atakuwa anaimarisha matumainin yake kusalia katika ligi kuu ya akina dada ikizingatiwa kuwa wote wameandikisha matokeo mbadala katika mechi chache zilizo pita.

Tukielekea utepeni mwa wikendi, itakuwa zamu ya ligi kuu ya wanaume kwa mara nyingine pale ambapo USIU itaialika Parklands ambao wanazogwa na tisho la kushuka daraja iwapo hawataibuka na ushindi. Kwa upande wao, baada ya kuandikisha ushindi dhidi ya Greensharks na kuenda kuipima nguvu nchini Uganda, USIU wanarejea huku wakihakikishia wafuasi wao kuwa wamenoa makali yao tayari kumkabili yeyote yule atakaye kuja mbele ya.

Kilele cha wikendi itakuwa wakati wa mechi ya watungulizi wetu katika magongo almaarufu Masters league. Mchuano utakuwa kati ya Impala Masters na Sikh Masters. Impala wanarejea ugani baada ya kupewa adhabu kali ya mabao manne kwa moja dhidi ya Armed Forces masters wakiongozwa na Col. Nahashon Randiek nayo Sikh wakiongozwa na gwiji Inderjit Matharu wanajitosa ugani baada ya ushindi dhidi ya Parkroad.

Ratiba ya mechi za Jumapili

Ligi Timu Saa Uga
PLM Kenya Police vs Western Jaguars 09:00 City Park
SLM Bungoma Farmers vs KCAU 10:00 Bungoma
SLW TUK-Women vs MSC-Women 11:00 City Park
SLM MMU-Men vs Nakuru 13:00 City Park
PLW KU-Women vs JKUAT-Women 15:00 City Park
PLM USIU-A vs Parklands 17:00 City Park
ML Impala Veterans vs Sikh Veterans 18:30 City Park

Kutoka meza ya waandishi pamoja na wapiga picha wa Magongo Kenya, tunawatakia wote watakao shiriki kwa njia moja au nyingine kufanikisha wikendi hii, kila laheri

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *